Kocha wa makipa klabu ya Yanga Razack Siwa amesema timu iko tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Ruvu Shooting ambao utapigwa kesho Alhamisi katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Akizungumza na Wanahabari leo katika Mkutano wa maandalizi kuelekea mchezo huo, Siwa amesema timu imepata wasaa mzuri wa kujiandaa wakati wa mapumziko ya michezo ya Kimataifa
Aidha Siwa amesema Yanga imedhamiria kushinda michezo yote iliyobaki, bado wako katika mbio za kuwania ubingwa kwani ligi bado haijamalizika
"Mapumziko ya wiki mbili tuliyopata yametusaidia kuiandaa timu vizuri kuelekea mechi za kukamilisha msimu. Kuelekea mchezo wetu wa kesho dhidi ya Ruvu Shooting wachezaji wapo kwenye hali nzuri"
"Kuhusu suala la ubingwa bado ligi haijaisha na tumejipanga kuhakikisha tunashinda mechi zetu na mwishoni tutaangalia tumepata nini," alisema Siwa
Nae mlinda lango Ramadhani Kabwili amesema pamoja na kuiheshimu Ruvu Shooting, wamedhamiria kushinda mchezo huo ili kuendelea kubaki katika mbio za kuwania ubingwa msimu huu
"Tunaamini utakuwa mchezo mzuri sana kwasababu bado tuna malengo ya kuchukua ubingwa, tunaiheshimu Ruvu Shooting lakini sisi kama wachezaji tupo tayari kwa mchezo," alisema Kabwili