Baada ya Yanga kudaiwa kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa Kaizer Chiefs Lazarus Kambole wengi wamekosoa usajili wa mshambuliaji huyo kwa kuangalia takwimu zake kule Afrika Kusini
Wapo wanaouliza maswali kuwa Yanga inawezaje kusajili mchezaji aliyefunga bao moja katika michezo 39 ligi kuu ya Afrika Kusini?
Lakini wasichofahamu wengi ni kuwa Kambole alisajiliwa na Kaizer Chiefs baada ya kufanya vizuri sana kwenye ligi kuu ya Zambia katika klabu ya Zesco United
Kambole alijiunga na Zesco United mwaka 2016, alifanya vizuri tangu wakati huo. Msimu wa 2018/19 aliibuka kuwa mfungaji bora, mchezaji bora wa msimu na mchezaji wenye nidhamu
Katika mechi 59 alizoitumikia Zesco United, aliweka kambani mabao 40
Kama ilivyo kwa wachezaji wengi wanapojiunga na timu mpya, zipo changamoto zinaweza kuwafanya wasitambe
Mfano ugeni wa ligi, kutokuwa na nafasi ya kucheza mara kwa mara au kubadilishiwa majukumu tofauti na walivyotumika awali
Luis Miquissone anayefanya vizuri sana na klabu ya Simba, aliwahi kusajiliwa na Mamelodi Sundowns lakini hakuna takwimu zozote zinazoonyesha mafanikio yake huko Afrika Kusini
Wakati Simba wanamsajili, alikuwa ametolewa kwa mkopo klabu ya UD Songo. Amekuja Tanzania, amekuwa mchezaji tegemeo
Kama Simba wangehangaika na takwimu zake huko Afrika Kusini, pengine wasingemsajili
Yanga wasingemsajili Bernard Morrison ambaye kwa sasa yuko Simba kama wangeangalia takwimu zake Afrika Kusini na DR Congo
Hawa akina Michael Sarpong, Fiston Abdulrazak walikuwa wachezaji hodari kwenye timu walizotoka lakini walipokuja Tanzania hali imekuwa tofauti
Mwaka juzi walisajiliwa akina Juma Balinya ambaye alikuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya Uganda, Issa Bigirimana, Patrick Sibomana, Sadney wote hawakuwa na wakati mzuri Yanga
Nani anamkumbuka Yikpe? Alisajiliwa na Yanga akitokea klabu ya Gor Mahia lakini akaachwa baada ya miezi sita
Alikwenda kucheza Arabuni, akafanya vizuri na hivi karibuni amesajiliwa na klabu ya Ligi Kuu huko Libya tena akisajiliwa kama mfalme
Hivi mnakumbuka takwimu za yule mshambuliaji Junior Lokosa aliyesajiliwa na Simba msimu huu kwa ajili ya michuano ya ligi ya mabingwa?
Yule alikuwemo kwenye kikosi cha Esperance kilichotwaa ubingwa wa Afrika miaka msimu wa 2018/19. Alitua Esperance baada ya kuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya Nigeria msimu mmoja nyuma
Hapa Tanzania hakufanikiwa kucheza hata mchezo mmoja wa mashindano, Simba wakimuondoa kimya kimya baada ya kuona hawafai
Timu makini kabla ya kufanya usajili wa mchezaji, zinafanya tathmini makini kwa kumfuatilia nyendo za mchezaji husika kwa muda mrefu
Wakati mwingine mashabiki tunawalaumu viongozi wetu wanakosea katika kusajili lakini kumbe ni sisi wenyewe presha yetu inapelekea wafanye makosa
Pia suala la kufanya vizuri au kushindwa ni la mchezaji mwenyewe, bahati mbaya hapa kwetu mashabiki tuna utamaduni wa kuweka matumaini makubwa sana kwao bila ya kuwapa muda wachezaji
Presha inakuwa kubwa zaidi pale wanapoanza kwa kusuasua, mwisho wa siku wanakosa nafasi ya kudhihirisha ubora wao
Upo ushahidi wa wachezaji wengi walioshindwa kutamba hapa nchini lakini baada ya kuondoka wakafanya vizuri