Sio siri tena Yanga iko mbioni kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa Kaizer Chiefs Lazarous Kambole kuimarisha safu yake ya ushambuliaji
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Yanga, Injinia Hersi Said alitua Afrika Kusini jana kwa ajili ya kukamilisha usajili huo
Inaelezwa mazungumzo ya Yanga na Chiefs kuhusu mchezaji huyo yalishafanyika kabla ya Injinia kukwea pipa
Kambole ni mmoja wa washambuliaji mahiri wanaotokea katika nchi ya Zambia
Mwaka 2019 Kambole alisajiliwa na Kaizer Chiefs akitokea klabu ya Zesco United iliyokuwa ikinolewa na George Lwandamina ambaye kwa sasa ni kocha wa Azam Fc
Chiefs walifanikiwa kumsajili Kambole baada ya kuwazidi ujanja wapinzani wao Orlando Pirates ambao pia walitaka huduma ya mchezaji huyo
Wengi wanaweza kubeza takwimu zake tangu alipojiunga na Chiefs, lakini haiwezi kuwa kipimo cha ubora wake
Huyu ni mchezaji ambaye mwaka 2019 alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa ligi kuu ya Zambia, pia akishinda tuzo hiyo katika klabu yake ya Zesco na tuzo ya mchezaji mwenye nidhamu
Moja ya changamoto alizokutana nazo katika klabu ya Chiefs, ni kutumiwa katika nafasi ambayo hakuwa akicheza awali
Tangu aliposajiliwa na Kaizer Chiefs, Kambole ametumika zaidi kama winga wakati asili yake ni mshambuliaji wa kati
Lwandamina aliwahi kumshauri kocha aliyetimuliwa Kaizer Chiefs Gavin Hunt kuwa ili aweze kunufaika na Kambole anapaswa kumtumia kama mshambuliaji wa kati
"Kambole ni hatari akiwa karibu na goli. Kuna wakati hata mimi (Lwandamina) niliwahi kujaribu kumtumia kama winga namba 7 na 11 kutokana na kasi yake lakini alishindwa. Nilipomrudisha eneo la ushambuliaji alifanya vizuri sana," Lwandamina alivyokaririwa na mtandao wa Kickoff
Naamini Yanga inakusudia kumsajili Kambole kama mshambuliaji na sio winga nafasi aliyotumika zaidi na Kaizer Chiefs
Huyu ni mshambuliaji anayeshikilia rekodi ya kufunga hatrik ya muda mfupi zaidi kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika
Alifanya hivyo msimu wa 2018/19 alipotumia dakika tano tu kufunga mabao matatu dhidi ya Eswatini