Jana Afisa Habari wa klabu ya Simba Haji Manara alibeza tetesi ziliokuwa zikimhusisha mlinzi wa kulia wa AS Vita Shabani Djuma kusajiliwa na Yanga
Manara alidai kuwa dau la mchezaji huyo ni dola laki tano, na alikuwa akiwaniwa na vigogo wa soka barani Afrika Mamelodi Sundowns, Al Ahly na hata TP Mazembe
Leo imethibitika pasipo na shaka kuwa Yanga imemsajili Djuma Shabani, Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM Injinia Hersi Said akisafiri DR Congo kukamilisha usajili huo
Sasa Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amempiga 'dongo' Manara aache kusemea timu nyingine akidhani haziwezi kufanya sajili kubwa kama walivyo wao
Aidha Bumbuli amesema Yanga wanasubiri amtaje mchezaji mwingine ghali ili wakamn'goe
Katika usajili wa kuelekea msimu ujao, Yanga imedhamiria kufanya sajili kubwa za wachezaji watano wa kigeni ambao watakuja kukiongezea nguvu kikosi cha kocha Nasreddine Nabi tayari kwa msimu ujao