Nyota waliowahi kutamba klabu ya Yanga wametaka wahusishwe katika usajili wa timu hiyo ili kupata wachezaji wenye uwezo na hadhi ya kuwatumikia mabingwa hao wa kihistoria
Kwa misimu miwili Yanga imesajili wachezaji wapya zaidi ya 20 hata hivyo bado kumekuwa na maoni kuwa wengi wa wachezaji hao, uwezo wao ni wa kawadia
Aidha idadi kubwa ya wachezaji waliosajiliwa kuanzia mwaka juzi wameachwa baada ya kuonyesha viwango visivyo vya kuridhisha
Beki wa zamani wa Yanga Bakari Malima 'Jembe Ulaya', amesema suala la usajili wa wachezaji wapya Yanga lisiwe la mtu mmoja, lishirikishe watu wengi ikiwa ni pamoja na kuwahusisha wakongwe hao walioitumikia Yanga kwa heshima kubwa
Aidha Malima ameeleza masikitiko yake kwa Yanga kutokuwa na mchezaji yeyote kwenye mbio za kuwania ufungaji bora ligi kuu akitaka nguvu kubwa kwenye usajili ielekezwe katika safu ya ushambuliaji
"Yanga wanatakiwa kuongeza watu wengine wenye uwezo wa kupachika mabao. Kuna matatizo sana sehemu ya ushambuliaji, ingawa katikati kidogo kunatakiwa kufanyike marekebisho, lakini mbele ni matatizo"
"Yalifanyika makosa makubwa sana kumuachia David Molinga. Yule ndiyo alionekana kama mzito kwa sababu hajacheza muda mrefu, lakini alikuwa ni mshambuliaji mzuri sana kama angepewa muda, sema mihemko ya mashabiki ikawaingia viongozi wakaachana naye. Hata kama hawatowaondoa mastraika waliopo, lakini watafute wengine," alisema Malima
Naye Ramadhani Kampira amesema kama hakutakuwa na umakini katika usajili, Yanga msimu ujao inaweza ikarudi pale pale.
"Mimi nawashauri watoe nafasi kwa wachezaji wa zamani ndiyo watafute wachezaji. Kuna wachezaji wazuri Zambia, DR Congo, lakini nani anakwenda kuwaangalia na kuwaleta. Bado sisi Yanga tuna tatizo kwenye ushambuliaji, hilo ndiyo kwanza lingekuwa kipaumbele kuliko mengine"