Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga Haji Mfikirwa amesema usajili unaotarajiwa kufanywa na timu hiyo utazingatia mapendekezo ya Kocha Mkuu Nasreddine Nabi na sio mtu mwingine
Aidha Mfikirwa amesema Yanga inakusudia kufanya usajili utakaolenga kufanya maboresho ya kikosi na sio kufanya usajili mpya wa timu nzima
Kumekuwa na tetesi nyingi zinazowahusisha baadhi ya wachezaji kusajiliwa na Yanga, Mfikirwa amesema usajili wao utafanyika kwa kuzingatia mapendekezo ya Mwalimu
Amesema wanasubiri ripoti ya Nabi kuona mapendekezo ya wachezaji ambao anawahitaji kwa ajili ya kuboresha kikosi chake kwa msimu ujao wa michuano itakayowakabili.
"Viongozi hatutapelekeshwa na maneno, tutafanya usajili kwa kufuata utaratibu ikiwamo kusubiri ripoti ya kocha wetu (Nabi), kwa kuona aina ya wachezaji ambao anaowahitaji kwa ajili ya kuboresha kikosi cha timu yetu kwa msimu ujao"
"Msimu uliopita tulifanya usajili bila kuwapo kwa Kocha Mkuu, ila msimu huu tutasajili wachezaji tukiwa na benchi la ufundi lililokamilika," alisema Mfikirwa
Kwa misimu miwili mfululizo, Yanga imekuwa ikifumua karibu kikosi chote na kusajili nyota wapya huku pia wakati wa dirisha dogo ikiongeza wengine, jambo ambalo limekuwa likiwagharimu kuweza kuzoeana mapema