Katika mahojiano na eFM mapema leo, Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM Injinia Hersi Said alikiri kuwa idara ya habari ya Yanga imekosa muunganiko mzuri
Hersi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, amesema mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji yataondoa changamoto zinazojitokeza
Yanga ina maofisa wawili wanaohusika na kuhabarisha Wanayanga katika masuala mbalimbali yanayoihusu klabu
Kuna Hassan Bumbuli ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano lakini pia yupo Antonio Nugaz ambaye ni Afisa Mhamasishaji
Kuna wakati kulitokea mgongano katika mgawanyo wa majukumu kabla ya vitengo vyao kutenganishwa
"Tunakiri kwamba muunganiko wa Idara yetu ya Mawasiliano sio mzuri. Kwa kuwa tunaelekea kwenye mabadiliko, changamoto hiyo itakwenda kumalizwa na mfumo mpya wa uendeshaji wa klabu,” alisema Hersi
Katika hatua nyingine, Injinia Hersi amesema sio vyema mafanikio ya klabu ya Yanga kulinganishwa na Simba kwani wao wamewazidi Simba katika nyanja zote
"Yanga hatuwezi kujipima mafanikio kwa kuiangalia Simba tumewazidi kwenye nyanja zote.Hatuwezi kuwa na mpango mkakati wa mafanikio ya kumuangalia Simba. Kwa hiyo Namungo naye akikaa pale juu, na sisi tujinasibu tunataka tuwe wazuri kama wao?"
Hersi amesema kwa wakati huu Yanga ina mipango yake ya kuimarisha timu
"Hii presha ambayo viongozi tunakutana nayo inasababishwa na mambo mawili. Kwanza ni matarajio makubwa ya mashabiki wa Yanga kwa timu yao. Yanga ni timu kubwa hivyo mashabiki wanatarajia kuiona ikishinda makombe. Lakini pili ni hili la kufananishwa na Simba ingawa kiuhalisia kwa sasa sisi tunapaswa kuimarisha timu yetu zaidi"