Michuano ya kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) inaendelea kutimua vumbi leo kwa mchezo mmoja wa robo fainali kupigwa mkoani Shinyanga
Mwadui Fc watakuwa nyumbani kuwakabili mabingwa wa kihistoria Tanzania, Yanga
Huu ni mchezo wa pili wa robo fainali ambapo juzi Biashara United waitangulia hatua ya nusu fainali baada ya kuichapa Namungo Fc mabao 2-0
Mshindi wa mchezo wa leo, atakutana na Biashara United katika mchezo wa nusu fainali
Yanga inapewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo ukilinganisha na wapinzani wao Mwadui Fc
Kwenye ligi Yanga wanashika nafasi ya pili na kimahesabu bado wako katika mbio za kuwania ubingwa wakati kwa upande wa Mwadui Fc, wao tayari wamejihakikishia kushuka daraja, msimu ujao watacheza ligi daraja la kwanza
Hata hivyo Yanga inauangalia mchezo huo kwa taswira tofauti. Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema watafanya makosa makubwa kama watadhani itakuwa rahisi kwao kupata ushindi kirahisi na kuingia nusu fainali
"Hakuna timu ndogo kwenye michuano hii. Timu zote zilizotinga robo fainali ni timu nzuri hivyo hatutawadharau wapinzani wetu eti kwa kuwa wameshuka daraja. Tunawaangalia Mwadui Fc kama moja ya timu zilizofanya vizuri sana kwenye michuano ya kombe la Shirikisho na ndio maana wako hapa," alisema Bumbuli
Yanga ilitua Shinyanga juzi wakitokea mkoani Singida ambao waliweka kambi ya siku tatu
Kikosi cha kocha Nasreddine Nabi kilifanya mazoezi yake ya mwisho jana katika uwanja wa CCM Kambarage
Yanga leo itamkosa kiungo mshambuliaji Saido Ntibazonkiza aliyerejeshwa jijini Dar es salaam kutibiwa majeraha aliyopata katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya JKT Tanzania uliopigwa mkoani Dodoma wiki iliyopita
Kikosi kilichokuwa Dodoma ndicho kilichosafiri Shinyanga kwa ajili ya mchezo huo utakaoanza saa kumi kamili Alasiri