Msimu wa ligi kuu 2020/21 unaelekea ukingoni na tayari tetesi za usajili katika klabu mbalimbali zimeanza kuvuma
Mkurugenzi wa uwekezaji GSM Injinia Hersi Said ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Yanga alishaweka wazi kuwa wataingia sokoni kwa nguvu kubwa kupata wachezaji wa kuimarisha kikosi zaidi
Mmoja wa wachezaji wanaohusishwa na Yanga ni kiungo mshambuliaji Ibrahim Ajibu Migomba ambaye kwa sasa anaitumikia klabu ya Simba
Misimu miwili nyuma, Ajibu alikuwa Mwananchi ambapo msimu wake wa mwisho aliweka rekodi ya kibabe kwenye ligi kuu ya Vodacom
Ajibu alitoa pasi za mabao 17 huku mwenyewe akiweka kambani mabao 7
Aliondoka akiwa mchezaji muhimu sana lakini bahati mbaya huko alikokwenda amekosa nafasi ya kucheza
Msimu huu Yanga imekabiliwa na changamoto katika eneo lake la ushambuliaji, usajili mkubwa utafanyika katika eneo hilo kwa kuongeza viungo washambuliaji pamoja na washambuliaji asili
Ajibu atakuwa mchezaji huru msimu utakapofika mwisho, je Wananchi watakuwa tayari kumpokea iwapo atasajiliwa?
Kwani yeye na Gadiel Michael waliondoka Yanga katika kipindi ambacho walikuwa wakihitajika sana. Wengi wanaamini hawakujali hisia za mashabiki wao ingawa inaweza kuwa walikuwa sahihi kufuata maslahi
Kimsingi sio tatizo kwa mchezaji kuondoka klabu moja kisha kurejea tena, muhimu ni vile anavyotimiza majukumu yake
Haruna Niyonzima alisajiliwa na Simba lakini baada ya mkataba wake kumalizika akarejea Yanga na Wananchi walimpokea vizuri