Mikiki mikiki ya ligi kuu ya Vodacom inaendelea leo kwa michezo miwili kupigwa mkoani Dodoma na kule Misungwi, Mwanza
Yanga wako Makao Makuu ya nchi Dodoma ambapo jioni ya leo wataumana na wenyeji wao JKT Tanzania katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Jamhuri
Gwambina Fc wao watakuwa wenyeji wa Namungo, dimba la Gwambina Complex
Ni mchezo mwingine muhimu kwa Yanga kusaka ushindi ambao utawafanya wawafikie watani zao Simba kwa alama
Yanga imekusanya alama 58 baada ya kushuka dimbani mara 28 ikiendelea kushika nafasi ya pili
Mabingwa hao wa kihistoria wametokea kule Ruangwa ambako walilazimishwa suluhu ya bila kufungana dhidi ya Namungo Fc katika mchezo ambao walifunga bao halali lililokataliwa na mshika kibendera
Jana kamati ya saa 72 ilitangaza kumfungia mshika kibendera huyo, Abdulaziz Ali kukosa mizunguuko mitatu ya mechi za ligi
Yanga inazihitaji alama zote tatu mkoani Dodoma leo kwani matokeo tofauti yanaweza kuwapa nafasi Azam Fc kupanda kwenye nafasi ya pili kama watashinda mchezo wao dhidi ya Biashara United hapo kesho
Mchezo utapigwa kuanzia saa kumi kamili alasiri dimba la Jamhuri ambalo msimu uliopita Yanga iliacha alama mbili kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1