Ukweli ni kwamba kama nchi tumekuwa tukijidanganya sana kuwa tumepiga hatua kubwa katika soka letu
Kipigo cha mabao 4-0 ambacho Simba wamekipata kutoka kwa Kaizer Chiefs ni ujumbe mzuri kwa Mamlaka zinazohusika na usimamizi wa soka nchini kuwa wafahamu hata siku moja, ujanja ujanja hauwezi kutufikisha popote
Chiefs walionekana kama under-dog kabla ya mchezo dhidi ya Simba kwa kuangalia nafasi wanayoshika kwenye msimamo wa ligi kuu ya Afrika Kusini
Wananchi hawa wa Afrika Kusini wanashika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi yao
Lakini kama uliwaangalia katika mchezo wao dhidi ya Simba, utagundua kuna tofauti kubwa ya ushindani baina ya timu hizo mbili
Chiefs walionekana kuwa timu iliyokamilika zaidi ya inayocheza kwa malengo tofauti na wapinzani wao
Ni ishara kuwa hata ligi yao ni yenye ushindani zaidi kwa kuangalia vile Kaizer Chiefs walivyocheza licha ya nafasi wanayoshika katika msimamo wa ligi
Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wadau wa soka hapa nyumbani kuwa baadhi ya timu zimekuwa zikitengenezewa mazingira ya kushinda huku nyingine zikitengenezewa mazingira ya kushindwa
Haya malalamiko hayakuanza leo, ni bahati mbaya sana wale wanaoyatoa wanachukuliwa kama ni kawaida yao kulalamikaย hivyo hakuna haja ya kuwasikiliza
Suala la waamuzi ni donda sugu, kila mara wamehusika kuathiri matokeo ya mechi
Lakini hakuna hatua zinazochukuliwa zaidi ya kuwafungia na kuwafungulia baada ya muda
Tusidanganyane; Mafanikio waliyopata Simba msimu huu katika michuano ya CAFCL, kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na changamoto ya corona ambayo ilisababisha nchi nyingi kusitisha shughuli za michezo
Hapa Tanzania aliyekuwa Rais wa awamu ya Tano hayati Dk John Magufuli hakuweka lock-down na aliruhusu shughuli za michezo ziendelee
Wenzetu nao sasa wamerejesha shughuli zao ingawa ni kwa tahadhari kubwa
Hivyo taratibu tumeanza kuwapisha na tutarejea katika nafasi yetu tunayostahili
Ili tuweze kufanikiwa kama nchi, tunapaswa kuwa na ligi yenye ushindani na yenye usawa kwa timu zote
Waamuzi wanapaswa kuchezesha mechi kwa kuzingatia sheria 17 za mpira wa miguu
Wasiingiliwe kuathiri maamuzi yao, iwe kwa kurubuniwa(rushwa) au kupewa maelekezo kuzipendelea timu nyingine kwa sababu za kishabiki, kisiasa au nyingine zozote
Wenye mamlaka ya usimamizi wa soka wasizidiwe na mapenzi ya vilabu wanavyo-vishabikia kwani jukumu lao ni kulinda maslahi ya mpira wa miguu Tanzania na sio maslahi ya klabu wanazozipenda
Waache klabu zijisimamie zenyewe uwanjani ili washindi wawe wale wenye haki na wanaostahili