Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amepania kwelikweli kuondoka na alama tatu kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Namungo Fc ambao utapigwa keshokutwa Jumamosi uwanja wa Majaliwa
Yanga imeweka kambi Mtwara kujiandaa na mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka kusini mwa Tanzania
Nabi ndiye aliyependekeza kikosi chake kiweke kambi Mtwara kutokana na utulivu wa mkoani huo ambapo anaamini atapata muda wa kuwaandaa vizuri vijana wake
Takwimu za matokeo ya nyuma dhidi ya Namungo, yamemfanya Nabi kuhitaji eneo tulivu kwa ajili ya maandalizi
Yanga bado haijaweza kupata ushindi kwenye ligi dhidi ya Namungo, matokeo ya mechi zote tatu zilizopita yakiwa sare
Msimu uliopita mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es salaam ulimalizika kwa matokeo ya sare ya mabao 2-2 kisha timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa pili uliopigwa Ruangwa
Msimu huu mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es salaam ukamalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1, mchezo wa Jumamosi utakuwa wa pili
Yanga ilipata ushindi dhidi ya Namungo msimu wa 2018/19 katika mchezo wa kombe la FA bao hilo likiwekwa kambani na Heritier Makambo
Wakati huo Namungo walikuwa wakishidriki ligi daraja la kwanza
Yanga inahitaji kushinda mchezo huo ili kuendelea kubaki katika mbio za kuwania ubingwa wa ligi kuu msimu huu