Tukio la jana linapaswa kuwa funzo kwa viongozi wa soka ambao wanadhani wana mamlaka ya kufanya lolote bila ya kujali hasara wanazo wasababishia wadau wengine
Mpira wa miguu ni mali ya mashabiki na wadau wanaohusika kibiashara, uamuzi wowote unaofanywa lazima uzingatie maslahi ya watu hawa kwani wao ndio sababu ya mchezo huo kuwepo
Kama mashabiki hawataenda uwanjani, hawatalipia vin'gamuzi vyao kuangalia runingani, au wataacha kushiriki katika shughuli yoyote ya kibiashara inayohusiana na soka, mchezo huu hautakuwa na maana
Ni wiki iliyopita tu mashabiki wa soka Barani Ulaya waliwashinda matajiri waliojaribu kuanzisha michuano mingine bila ya kuwashirikisha
Umoja wao ulipelekea jaribio hilo likafa ndani ya saa 24 tu
Kilichofanywa na Yanga jana ni kutetea maslahi ya mashabiki wa soka ambao walilipa viingilio kushuhudia mchezo kuanzia saa 11 jioni
Kila shabiki aliyekwenda uwanjani alikuwa akifahamu mchezo unachezwa saa 11
Ndivyo walivyotaarifiwa kwa takribani mwezi mzima, kila mtu akajipanga katika muda huo
Lakini masaa mawili kabla ya mchezo, likatolewa tamko la kubadilisha muda wa mchezo tena bila ya kuwashirikisha wadau vilabu (Yanga haijashirikishwa) na mashabiki
Lazima jambo hili liwe na gharama ya kulipa kwa wale waliolifanya ili siku nyingine waliopewa mamlaka ya kusimamia soka waheshimu kanuni walizozitunga wao wenyewe
Yanga ina kila sababu ya kudai ipewe alama tatu baada ya Simba kutotokea uwanjani jana saa 11 kwani ndio muda ambao mchezo huo ulipaswa kuchezwa
Zipo sababu za mchezo kuahirishwa ambazo zimeainishwa kikanuni lakini hata TFF katika taarifa yao ya kusogeza muda wa mchezo mbele hawakutaja nini kilisababisha
Maagizo kutoka Wizarani haiwezi kuwa sababu walipaswa kubainisha maagizo hayo ni yepi, yalitolewa na nani na je yapo katika zile sababu ambazo zinaweza kupelekea mchezo kuahirishwa?
Isije ikawa kuna mtu mmoja au kikundi cha watu kwa utashi au maslahi yao binafsi tu wakatoa agizo mchezo huo usogezwe mbele bila ya kujali hasara wanayokwenda kuwasababishia mashabiki na wadau wengine
Kuna watu walikuwa tayari na tiketi za safari ya kurejea makwao baada ya mchezo kumalizika
Jambo jema ni kuwa hata TFF wanafahamu FIFA hairuhusu Serikali kuingilia masuala ya soka, nje ya utaratibu ambao sio shirikishi
Yanga ina haki ya kupewa ushindi baada ya Simba kuingia mitini na kama TFF hawatakuwa tayari kuwapa ushindi basi shauri hili ni vyema walipeleke huko huko FIFA ili kama nchi tulipe gharama ya makosa ya wale tuliowapa mamlaka ya kusimamia soka letu
Labda tukipewa adhabu na FIFA baadae hatutakuwa tayari kuwapa mamlaka watu ambao hawana uwezo wa kusimamia mchezo wa mpira wa miguu kwa maslahi mapana ya walio wengi