Makocha Nasreddine Nabi (Yanga) na Didier Gomes (Simba) kwa mara ya kwanza kesho Jumamosi wataonja radha ya dabi ya Kariakoo watakapo-ziongoza timu zao katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom ambao utapigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Wakati Gomes akiwa ameiongoza Simba kwa takribani michezo 20, huu utakuwa mchezo wa tatu kwa Nabi aliyetua mwezi uliopita kuchukua nafasi ya Kocha Cedric Kaze
Katika michezo yake miwili, Nabi ameshinda mchezo mmoja na kupoteza mmoja. Alipoteza mchezo dhidi ya Azam Fc lakini akapata ushindi mchezo dhidi ya Tanzania Prisons na kuipeleka Yanga robo fainali ya michuano ya kombe la Shirikisho la Azam
Katika makocha wanaofundisha hapa Tanzania, Nabi ndiye kocha mwenye CV kubwa zaidi. Kocha huyu raia wa Tunisia, ana leseni ya UEFA Pro ambayo inamuwezesha kufundisha timu yoyote duniani
Yaani Nabi anaweza kupewa mikoba ya kuinoa klabu kama Real Madrid, Fc Barcelona, Manchester United, Liverpool au hata akachukua kibarua cha Mikel Arteta pale Arsenal
Ni kocha aliyeiva kimbinu, mechi ya kesho dhidi ya Simba ndio mtihani wake kwa kwanza nchini, mchezo huo utamfanya azungumzwe zaidi au la
Nabi amepania kuishangaza Simba siku ya kesho. Pamoja na kuwa na muda mfupi tangu akabidhiwe timu, amesema hatakubali kupoteza mchezo huo kutokana na ufundi aliowapa wachezaji wake tangu kumalizika kwa mchezo wao wa Kombe la FA dhidi ya Tanzania Prisons
Nabi amefichua kuwa, kuelekea mchezo huo hana wasiwasi wowote kwani amewapa wachezaji wake mbinu mbadala zitakazowasaidia kuibuka na ushindi.
Uzuri ni kuwa Nabi aliwafahamu Simba kabla hajatua Yanga. Alikuwa kocha wa Al Merrikh na aliiongoza timu hiyo katika mchezo wa ligi ya mabingwa uliopigwa kule Sudan na timu hizo kutoka suluhu ya bila kufungana
Baada ya mchezo huo Nabi aliachana na Al Merrikh ambapo walipokuja jijini Dar es salaam ndio wakafungwa mabao 3-0
Mkufunzi huyo mwenye uraia pacha wa Ubelgiji na Tunisia, amesema amewafuatilia Simba wakicheza mechi mbalimbali za ligi pamoja na michuano ya kimataifa, hivyo amewasoma vizuri mbinu na mifumo wanayotumia na tayari amewaandaa watu maalumu wa kuwadhibiti nyota wao
"Hakuna ubishi kwamba tunakwenda kucheza na timu bora kwenye ligi ya Tanzania, timu ambayo inaongoza ligi, lakini wajue kwamba Yanga ni timu kubwa na inahistoria yake kwenye soka la Tanzania, ninachofanya ni kuwapa mbinu ambazo zitawaweka katika wakati mgumu wapinzani wakati huo huo tukitengeneza mashambulizi ambayo yatakuwa na madhara makubwa kwao," alisema Nabi
Kocha huyo alisema anatambua kwamba endapo watapoteza mchezo huo watakuwa wametoa nafasi kubwa kwa wapinzani wao Simba kutwaa ubingwa, hivyo kwa mbinu alizopanga kuzitumia anaamini watapata ushindi na wachezaji wake wamempa matumaini makubwa ya kushinda mchezo huo kutokana na kushika haraka kile anacho waelekeza mazoezini