May 08 Wananchi wana jambo lao pale dimba la Benjamin Mkapa, wenyewe wanasema watachinja Mnyama!
Ni mchezo wa ligi kuu unaozikutanisha timu mbili zenye historia kubwa na soka la Tanzania, Simba na Yanga
Hii inaweza kuwa mechi kubwa zaidi ya dabi katika ukanda wa Afrika Mashariki, umaarufu wake pia ukivuma katika kona za bara la Afrika
Taswira sahihi kuhusu mchezo huu unaweza kuipata kupitia shamrashamra zake. Ni mchezo unaogusa kila familia
Siku ambayo mchezo huo hupigwa huingia katika historia na zipo nyakati timu inaweza kutopenda mchezo huo uchezwe tarehe fulani kutokana na historia ya matokeo ya nyuma
Nakumbuka mchezo wa duru ya kwanza uliopigwa Novemba 07, awali ulipangwa kupigwa Oktoba 18 lakini ukasogezwa mbele katika mazingira ya kutatanisha
Baadae akasikika msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara kupitia chombo kimoja cha habari akisema kuwa wao Simba hawapendi kucheza mechi zao na Yanga katika tarehe yoyote yenye namba nane kwani mara nyingi huwa 'hawatoki'
Hata mchezo huo ulipopigwa Novemba 07 na kumalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1, wapo walioamini kuwa kama ungepigwa Oktoba 18, wasingetoka kweli maana katika mchezo huo walirudisha bao kwenye dakika ya 87
Manara pia akafichua kuwa kwa upande wao Simba mchezo wowote unaopigwa katika tarehe yenye namba mbili ushindi huwa ni wao
Sehemu ya video ya mahojiano yake imesambaa katika mitandao ya kijamii, kwa mujibu wa kauli yake, ni kuwa May 08 hawatatoka!
Huo ni upande wa pili wa taswira ya mchezo wa watani wa jadi kwani pia hugubikwa na mambo mengi ya nje ya uwanja
Lakini naamini Yanga wanaweza kushinda mchezo huu sio kwa sababu umeangukia kwenye tarehe yenye namba nane, bali ni kutokana na maandalizi na uhitaji wa alama tatu
Ili kuendelea kubaki katika mbio za ubingwa msimu huu, Yanga inazihitaji alama zote tatu siku ya Jumamosi kuliko watani zao Simba ambao wana mechi mbili za viporo pia
Lakini pia ushindi kwa Yanga ni matokeo yatakayo 'iheshimisha' Yanga huku mtaani
Ukisikiliza redio, ukitizama TV na hata kusoma Magazeti utaona Simba inapewa nafasi ya kushinda kutokana na mafanikio waliyopata kwenye michuano ya ligi ya mabingwa
Watu hawana hata muda wa kuangalia takwimu za michezo mitano iliyopita ambapo Yanga imefungwa mara moja tu na Simba na yenyewe ikishinda michezo miwili na kutoka sare mechi mbili
Huu ni mchezo ambao wachezaji wa Yanga watahitaji kudhihirisha kuwa wako imara na watawafikishia salamu wale wanaowachukulia 'poa'
Kwao hii ni vita kamili, hakika kwa aina ya maandalizi wanayofanya kule Kigamboni, hawataiomba heshima bali wataichukua kwa mikono yao