Beki ghali zaidi nchini Bakari Nondo Mwamnyeto alianza majukumu yake vyema katika kikosi cha Yanga akicheza karibu mechi zote za duru ya kwanza
Hata hivyo nyota huyo ni kama alipungua makali tangu kuanza kwa duru ya pili
Kocha Juma Mwambusi wakati akikaimu nafasi ya kocha mkuu, alifanya mabadiliko eneo la walinzi wa kati kwa kuwatumia Abdallah Shaibu Ninja na Dickson Job ambao walifanya vizuri katika michezo mitatu waliyocheza pamoja
Mapema mwaka huu, Mwamnyeto alipata msiba wa kufiwa na mchumba wake aliyepata changamoto wakati wa kujifungua na bahati mbaya pia akampoteza mtoto
Huu ulikuwa msiba mkubwa sana kwake na kwa hakika ulimuathiri kwa kiasi kikubwa na hivyo kushindwa kutimiza majukumu yake vyema
Kuna wakati uongozi wa Yanga ulimpa beki huyo mapumziko ili aweze kutuliza akili yake
Naamini kwa kiasi kikubwa jambo hili lilimuathiri sana Mwamnyeto, yeye ni binadamu kama tulivyo sote hasa tunapokumbana na nyakati ngumu, wakati mwingine tunahitaji muda kusahau
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Mwamnyeto amemuomba M/Mungu amsaidie aweze kusahau machungu yote na aweze kurejea katika hali yake ya kawaida
"Mungu unijalie yote yaliyopita nisifikirie, nipe nguvu ya kusonga mbele. Mawazo yote ya huzuni yaishe na kurudi kazini salama. Hakika nitayasahau mambo ya nyuma japo ni ngumu mara moja lakini naamini nitarudi katika hali yangu salama"