Wakati Nadir Haroub 'Cannavaro' anastaafu kuitumikia Yanga, jezi namba 23 aliyoitumia miaka yote 12 alimkabidhi beki Abdallah Shaibu 'Ninja' ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 20 tu
Nadir alijiridhisha kuwa ni mchezaji anayeweza kurithi mikoba yake na kupata mafanikio katika kikosi cha Yanga, ni Ninja
Wakati huo Ninja alionekana kama mchezaji wa kawaida sana. Lakini msimu mmoja baadae akapata nafasi ya kusajiliwa na klabu moja barani Ulaya ambayo ilimtoa kwa mkopo kule Marekani kunako klabu ya LA Galaxy aliyokuwa akicheza mkali Zlatan Ibrahimovic


Baada ya mkopo wake wa miezi sita kumalizika, Ninja alirejea barani Ulaya lakini kutokana na changamoto ya corona, alilazimika kurejea nchini na ligi ziliposimama ndio mpango wa kurudi tena Ulaya ukawa umekwama
Shaibu alirejea Yanga mwishoni mwa msimu uliopita akifanya mazoezi na kikosi kilichokuwa kikinolewa na Luc Eymael
Dirisha la usajili lililofunguliwa Yanga ikamrejesha kundini. Awali hakuwa chaguo la kwanza pengine kwa kuwa hakupata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza
Akafanya vizuri kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi na baadae Juma Mwambusi alipokabidhiwa timu, akamrejesha katika kikosi cha kwanza
Leo Ninja anawapa amani mashabiki wa Yanga kwani wanaamini safu ya ulinzi iko salama sana wanapomuona uwanjani
Ninja wa sasa amekomaa, anatumia akili, nguvu na maarifa katika kutimiza majukumu yake
Sio beki unayeweza kumpita kirahisi. Washambuliaji hawapendi kukutana na beki aina ya Ninja kwani ni kisiki kwelikweli
Mshambuliaji wa Azam Fc Prince Dube pamoja na kufunga bao pekee katika mchezo dhidi ya Yanga, alimtaja Ninja kuwa mchezaji aliyemvutia zaidi kwenye safu ya ulinzi ya Yanga
Wanayanga wanausubiri kwa hamu mchezo wa dabi May 08, kwani uwepo wa Ninja katika safu ya ulinzi umeongeza matumaini kuwa hakutakuwa na njia nyepesi ya kupita kwa washambuliaji wa Simba