Kiungo mwandamizi wa Yanga Haruna Niyonzima amewataka mashabiki wa timu hiyo waendelee kuiunga mkono timu yao pasipo kukata tamaa kwani bado wana nafasi ya kufanya vizuri
Baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Azam Fc mwishoni mwa wiki, mashabiki wengi wameonyesha kukata tamaa wakiamini mabingwa hao wa kihistoria wameondoshwa kwenye mbio za ubingwa msimu huu
Niyonzima amesema matokeo hayo yamewaumiza sana hata wao wachezaji lakini jambo muhimu hawapaswi kukata tamaa kwani bado msimu haujamalizika
"Matokeo mabaya ni kweli yanaumiza hata sisi wachezaji hakuna anayefurahia kuona timu yake haipati matokeo mazuri, tunaumia sana lakini hatuna jinsi, cha msingi tunaangalia mechi zijazo tufanye vizuri"
"Nawaambia wachezaji wenzangu wasivunjike moyo kwani mpaka sasa hakuna mwenye uhakika wa ubingwa"
"Najua mashabiki wetu wanaumia sana kuona timu haifanyi vizuri lakini wajue Mungu huenda kuna kitu kikubwa ametuandalia huko mbele, habari za kulalamika hadi kupitiliza sio vizuri zinatuvunja moyo wachezaji," alisema Niyonzima
Kwa sasa Yanga inajiandaa na mchezo wa kombe la FA dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa Ijumaa, uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga
Baada ya mchezo huo Yanga inakabiliwa na mchezo wa pili wa dabi dhidi ya watani zao Simba utakaopigwa May 08 uwanja wa Benjamin Mkapa