Kwa hakika mlinda lango Farouk Shikhalo amekuwa na kiwango kisichotabirika msimu huu
Baada ya kucheza mechi moja tu duru ya kwanza VPL, Farouk aliaminiwa na akafanya vizuri sana kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi kule Visiwani Zanzibar
Aliibuka kuwa mlinda lango bora wa mashindano
Ni kiwango alichoonyesha kule Zanzibar ambacho kilirejesha imani ya benchi la ufundi kwake na hivyo kurejeshwa kuwa kipa namba moja dhidi ya Metacha ambaye pia alikumbana na changamoto baada ya ujumbe alioachia kwenye mitandao ya kijamii akiwaaga mashabiki
Lakini ni wazi Farouk bado hajafanikiwa kurejea katika kile kiwango alichojiunga na Yanga. Amekuwa akifanya makosa mengi

Jana alifungwa bao na Prince Dube kutoka umbali wa mita 35. Pamoja na kumsifu Dube, lakini ni mpira ambao mlinda lango mzuri alipaswa kuokoa
Hata baada ya mchezo Shikhalo alionekana kuwa na huzuni sana kwa kuwa anafahamu hakupaswa kufungwa goli lile
Mkufunzi wa makipa Razak Siwa ana kazi ya kufanya kuhakikisha mlinda lango huyu wa zamani wa timu ya Taifa ya Kenya anarejea katika makali yaliyomfanya awe sehemu ya kikosi cha Kenya kilichoshiriki Afcon 2019 kule Misri
Lakini pia Siwa anao Metacha na Kabwili ambao anaweza kuwatumia ili kumpa changamoto Shikhalo