Kimahesabu itakuwa ngumu kwa Yanga kushinda ubingwa wa ligi kuu baada ya kipigo dhidi ya Azam Fc hapo jana, ukweli utabaki kuwa hivyo
Kwa sasa mapambano ya ligi kuu ni kuhakikisha Wananchi hawamalizi chini ya nafasi ya pili ili kuwania kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa msimu ujao
Lakini ipo nafasi ya kwenye michuano ya kombe la FA, Ijumaa ya wiki hii Yanga ikitarajiwa kusafiri kule Sumbawanga kuikabili Tanzania Prisons
Ni mchezo mwingine mgumu kwa Yanga lakini ushindi utawapeleka robo fainali ya michuano hiyo ambayo msimu uliopita walitolewa hatua ya nusu fainali na watani zao Simba kwa kukubali kipigo cha mabao 4-1
Msimu huu Yanga haijaweza kupata ushindi dhidi ya Tanzania Prisons mechi zote mbili kwenye ligi zikimalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1
Lakini katika mchezo huo lazima mshindi apatikane, kama kutakuwa na sare changamoto ya mikwaju ya penati itatumika
Yanga iliweka malengo makubwa msimu huu, kwa hakika itakuwa fedheha kama mabingwa hao wa kihistoria hawatafanikiwa kupata ushindi dhidi ya Prisons na kutinga robo fainali