Mkufunzi wa makipa klabu ya Yanga Razak Siwa amesema wako tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Azam Fc ambao utapigwa kesho Jumapili katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Siwa aliwakilisha benchi la ufundi la Yanga leo kwenye Mkutano wa mechi ambao huwakutanisha walimu na manahodha wa timu kuelezea maandalizi ya mchezo unaofuata baina yao
Baada ya kushinda michezo miwili mfululizo, kocha huyo raia wa Kenya amesema morali ya wachezaji iko juu na hadhani kama Azam Fc wataweza kuwazuia hapo kesho
"Hakuna wa kutuzuia, kama wao wametoka sare mchezo uliopita sisi tulishinda mechi mbili mfululizo, tumefanya maandalizi ya kutosha, morali ya wachezaji iko juu tayari kwa mchezo huo"
"Wachezaji wako sawa kwa mchezo majeruhi ni wawili tu Balama Mapinduzi na Tuisila Kisinda yeye ni 50 kwa 50," alisema Siwa
Yanga ndio mwenyeji wa mchezo huo utakaopigwa kuanzia saa mbili na robo usiku katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam