Mlinzi wa kati Dickson Job aliyesajiliwa na Yanga katika usajili wa dirisha dogo mwezi Januari, alipata mapokezi mazuri baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo wa kwanza kuitumikia Yanga dhidi ya Biashara United
Job alilazimika kusubiri kwa takribani miezi mitatu kucheza mchezo wake wa kwanza akiwa na Yanga kutokana na majeruhi yaliyokuwa yakimsumbua
Beki huyo aliyekabidhiwa jezi namba tano iliyokuwa ikitumiwa na mkongwe Kelvin Yondani, ameushukuru uongozi na mashabiki kwa kumvumilia katika kipindi chote alichokuwa majeruhi
"Napenda kutanguliza shukrani zangu za dhati kwa uongozi,mashabiki pamoja na wanachama wote wa yanga. Niwashukuru kwa uvumilivu na sapoti yenu kwa kipindi chote nilichokuwa majeruhi"
"Kwa mara ya kwanza juzi nimepata nafasi ya kuwatumikia na ni matumaini yangu mlifarijika kwa point tatu muhimu za juzi. Tutaendelea kupambana kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi msimu huu," Job aliandika ujumbe katika ukurasa wa mtandao wake wa kijamii