Jana Yanga ilikuwa na umiliki mkubwa wa mpira pengine kuliko mechi nyingi walizocheza karibuni. Mipira mingi ilipita katika eneo la kiungo ambalo alikuwepo Carlinhos na Mukoko na wakati mwingine Saido akishuka chini
Kumekuwa na mijadala kuwa Yanga imekuwa ikipata tabu kutengeneza nafasi kwa kuwa haina kiungo mchezeshaji
Pengine ni kwa sababu Carlinhos alikosekana kwa muda mrefu kutokana na majeraha na ile adhabu ya kadi nyekundu
Aidha makocha wote waliopita walikuwa hawamwamini sana Carlinhos kucheza eneo la kiungo cha uchezeshaji, hivyo muda mwingi alitumika kama kiungo anayetokea upande wa winga
Ujasiri wa kocha Juma Mwambusi jana umempa taswira ya kile kilichokuwa kikikosekana wakati Carlinhos anatumika kama winga
Pamoja na uwezo wake mkubwa wa kupiga mipira ya adhabu, Carlinhos ni fundi sana eneo la kiungo

Hana mambo mengi anapopata mpira, yeye kazi yake ni kupokea na kuupeleka mpira eneo sahihi tena kwa wakati sahihi
Pasi nyingi alizokuwa akipiga ni kuelekea mbele, ni mara chache sana utamuona akirudisha mpira nyuma
Uwezo wake mkubwa wa kupiga pasi ndefu ni faida kwani anaweza kuupeleka mpira eneo lolote akiwa popote
Carlinhos ni mchezaji wa daraja la juu sana, usibabaishwe na umbo lake kwani miguu yake ina nguvu na kichwani mwake kuna akili 'mingi' ya soka
Pengine wakati mwingine Mwambusi ajaribu kuwatumia yeye, Fei Toto na Mukoko pamoja na Carlinhos apewe uhuru wa kucheza popote (free role)
Hakika anaweza kuwa na madhara zaidi