Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga Juma Mwambusi amesema kuwa kikosi chake kiko tayari kuondoka na alama zote tatu katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Biashara United ambao utapigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Akizungumza katika Mkutano maalum wa maandalizi ya mchezo huo, Mwambusi amesema wamefanyia kazi changamoto zote zilizojitokeza katika mchezo uliopita
Aidha amebainisha kuwa dhumuni la Yanga ni kuhakikisha wanashinda kila mechi katika michezo 10 iliyobaki
"Tumeshafanyia Kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo uliyopita na tupo tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya Biashara United, mkakati wetu katika mechi kumi (10) zilizobakia ni kuvuna alama tatu (3) kwenye kila mchezo," amesema Mwambusi
Naye kiungo wa Yanga Haruna Niyonzima amesema wachezaji wote wamepania kusahihisha makosa yaliyojitokeza katika michezo iliyopita
"Hakuna Mchezaji wa Yanga anafurahia matokeo mabaya ambayo tunapata, yanayoongewa kuhusu wachezaji tunayasikia na yanatuumiza sana"
"Tumeshafanya makosa, hatutaki kurudia makosa tena. Huu ndio muda wa wanayanga kushikamana ili tuweze kukaa sawa, kupitia mchezo dhidi ya Biashara United tunahitaji kushinda ili kurejesha hali ya ushindi ndani ya timu ili morali irejee, wanayanga tunitaji sapoti yenu kesho," amesema Niyonzima