Baada ya hapo jana Mahakama ya Kinondoni kupitia Baraza la Ardhi na Nyumba kuipa Simba siku 14 kulipa deni la Tsh. Mil 77 kama fidia kodi ya ardhi, kuna taarifa imesambazwa kuwa Yanga pia ina deni kubwa la ardhi taarifa hiyo ikitumika kuaminisha umma kuwa Simba wameshitakiwa kwa lengo la kukomolewa
Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amezungumzia taarifa hiyo ambapo licha ya kukiri kuwa ni kweli wana deni la ardhi, lakini ametoa ufafanuzi kwa nini wao hawajashtakiwa kama ilivyo kwa watani zao Simba ambao kama hawatalipa deni lao ndani ya siku 14, wanaweza kupoteza uwanja wao wa Mo Simba Arena
Bumbuli amesema Yanga ina utaratibu wa kulipa madeni ya ardhi kwa awamu na ndio maana wao hawajashtakiwa
"Ni kweli tuna deni la ardhi na hilo lipo wazi kitambo. Tofauti yetu na wao, kila kitu kwao watasingizia wanakwamishwa uwekezwaji. Sisi tunalipa deni hilo, ndio maana hatujashitakiwa kama wao. Nashangaa wanataka kufunika deni lao kwa mgongo wetu, walipe tu," alisema Bumbuli