Jumamosi Yanga itashuka uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya mchezo mwingine wa ligi kuu dhidi ya Biashara United
Ingawa kwa macho ya kawaida inaonekana ni vigumu sana kwa Yanga kushinda ubingwa mbele ya watani zao Simba ambao mafanikio waliyopata kwenye michuano ya ligi ya mabingwa ni kama yamewaongezea moto, Wananchi hawapaswi kukata tamaa
Yanga bado iko kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na alama 51, alama mbili zaidi ya Simba inayoshika nafasi ya pili ikiwa na alama 49 huku wakiwa na michezo mitatu ya viporo
Jambo muhimu kwa Yanga ni kuhakikisha haifanyi makosa zaidi ya kudondosha alama hasa katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Njia pekee ya kuendelea kubaki katika mbio za ubingwa ni kushinda michezo yote iliyobaki ukiwemo mchezo dhidi ya Simba May 08
Nahodha wa Yanga Lamine Moro amewahakikishia mashabiki kuwa wachezaji hawajakata tamaa na hesabu zao sasa ni kushinda michezo inayokuja mbele yao
Ni kazi ngumu lakini inawezekana. Yanga ilishinda michezo mingi kwenye duru ya kwanza, kama wachezaji watarudisha ile morali waliyokuwa nayo wakati ule wanaweza kufanya vizuri
Sapoti ya mashabiki pia ni jambo muhimu. Ni kuwa, timu imepita katika kipindi kigumu tu, shabiki wa kweli ni lazima awe na timu yake katika vipindi vote
Wakati ambao timu haifanyi vizuri sapoti ya mashabiki ndio inahitajika zaidi ili kuwainua na kuwapa moyo
Wadhamini (GSM) na viongozi pia wanapaswa kuungwa mkono kwa jitihada zao za kuirudisha Yanga mahali pake
Pamoja na changamoto ya matokeo ambayo Yanga inapitia, lipo jambo la kujivunia kuwa timu imeimarika ukilinganisha na msimu uliopita
GSM wamejitosa kusajili wachezaji wazuri, ingawa yawezekana wapo baadhi wameshindwa kufikia matarajio ya wengi
Lakini haliwezi kuwa kosa la wawekezaji, wakati mwingine usajili ni bahati nasibu, mchezaji anaweza kufanikiwa au kufeli
Kubeza juhudi zilizofanyika ni kuwavunja moyo waliojitolea fedha zao kuwapa furaha Mamilioni ya Watanzania wanaoiunga mkono Yanga
Yanga hii itaendelea kuimarishwa pale msimu utakapomalizika, ni wazi wapo wachezaji wataachwa na wengine kusajiliwa