Nadhani kwa sasa Wanachama na Mashabiki wa Yanga hawapaswi kuwaweka kwenye presha viongozi wao, waache timu imalize msimu
Hapa yapaswa kukubaliana kuwa ujenzi wa timu imara sio jambo la siku moja. Juma Mwambusi ni kocha wa tatu kuinoa Yanga msimu huu baada ya Zlatko Krmpotic aliyekuwa akisaidiana nae na baadae Cedric Kaze
Pamoja na kuwa na lengo la kushinda ubingwa, Yanga inahitaji kujengwa kuwa imara, hii sio kazi ya siku moja
Wachezaji wengi waliosajiliwa ni wazuri lakini ni wazi wanahitaji muda zaidi kuweza kuelewana kitimu
Sio sawa kwa Yanga kuifananisha na Simba ambayo timu yao iko pamoja kwa takribani misimu mitatu
Simba wanaonekana kuwa bora kwa sababu wamekiweka kikosi chao pamoja kwa muda mrefu
Aidha hata aina ya sajili wanazofanya sasa ni kuboresha maeneo yanayoonekana kuwa na mapungufu tu
Kwa Yanga msimu huu ndio wa kwanza. Robo tatu ya wachezaji katika kikosi ni wapya tena wengine hawana zaidi ya miezi sita tangu waliposajiliwa
Makocha wote watakwambia wanahitaji muda kutengeneza timu. Bahati mbaya msimu huu umekumbwa na changamoto ya corona na hivyo hata wachezaji waliosajiliwa, wengine hawakuwa wakicheza baada ya ligi katika nchi walizokuwepo kufutwa
Zipo athari za mchezaji kutocheza kwa muda mrefu, tumeona baadhi ya wachezaji viwango vya vya sasa ni tofauti sana na viwango walivyokuwa navyo mwanzoni mwa msimu
Naamini msimu huu ukimalizika, viongozi watakuwa na muda mzuri wa kufanya tathmini na kuboresha maeneo yaliyoonekana kuwa na mapungufu na sio kufanya tena usajili wa timu nzima
Usajili wa timu nzima kila msimu sio njia sahihi ya kujenga timu imara