Kocha wa makipa klabu ya Yanga Razak Siwa amesema magolikipa watatu aliowakuta wana uwezo mzuri jukumu lake ni kuwasaidia kuondoa changamoto zinazowakabili
Juzi uongozi wa Yanga ulimtambulisha kocha huyo wa zamani wa Bandari Fc ya Kenya kushika majukumu yaliyoachwa na Niyonkuru
Siwa amewahi kuwa kocha wa makipa Yanga kwa misimu miwili kuanzia 2012/13

"Sina shida kabisa na makipa waliokuwapo sasa Yanga, wana uwezo mkubwa, kuna vitu ambavyo wanavikosa na mara nyingi nimepata kushuhudia mechi walizocheza na kuona makosa wanayoyafanya, nina imani nitawasaidia na kufikia malengo yetu," alisema Siwa
Siwa ameeleza kuridhishwa na mazingira ya kambi ya timu ya Yanga kule Kigamboni na ana matumaini makubwa kuwa kwa kushirikiana na wenzake ndani ya benchi la ufundi, wanaweza kutimiza malengo yaliyowekwa
"Nina imani kubwa Yanga ina nafasi ya kuchukuwa ubingwa endapo tutaungana kwa pamoja na kuhakikisha kila mechi iliyopo mbele yetu tunahitaji kupata ushindi bila kumfikiria anayetukimbiza ameshinda bao ngapi au amepoteza michezo yake"
Kabla ya kutua Yanga, Farouk Shikhalo aliwahi kufanya kazi na Siwa wakati yuko klabu ya Bandari Fc
Kipa huyo aliibuka kuwa mlinda lango bora wa ligi kuu ya Kenya kwa misimu miwili mfululizo huku akipata nafasi ya kujumuishwa katika timu ya Taifa ya Kenya iliyoshiriki fainali za Afcon 2019 zilizofanyika Misri
Wengi wana matumaini makubwa kuwa Siwa atamrejesha Shikhalo katika ubora wake aliokuwa nao misimu miwili nyuma