Hivi karibuni bosi anayehusika na masuala ya usajili klabu ya Kaizer Chiefs ya nchini Afrika Kusini, Walter Steenbok alitembelea klabu ya Yanga kujifunza pamoja na kuanzisha ushirikiano na Yanga hasa kwenye soka la vijana
Lakini pia imebainika kuwa klabu ya Kaizer Chiefs inawawania nyota wawili wa Yanga, Wacongomani Tuisila Kisinda na Mukoko Tomombe
Kisinda na Mukoko walitua Yanga katika usajili wa dirisha kubwa August 2020 wakitokea klabu ya AS Vita
Inaelezwa Kaizer Chiefs pia ilikuwa ikiwawania wachezaji hao lakini ikazidiwa ujanja na Injinia Hersi Said, Mkurugenzi wa uwekezaji GSM ambaye alisafiri DR Congo kumalizana na AS Vita iliyokuwa ikimmiliki Mukoko na klabu ya Meneama Fc iliyokuwa ikimmiliki Kisinda
Kama ilivyo Yanga, Chiefs wanaimarisha kikosi chao katika jitihada za kuwania ubingwa wa ligi kuu ya Afrika Kusini wakiukosa kwa misimu mitano sasa wakishuhudia ukichukuliwa na Mamelodi Sundowns
Mukoko na Tuisila wote walisaini mikataba ya miaka miwili kila mmoja wakati wanasajiliwa na Yanga, hivyo mwishoni mwa msimu bado watakuwa na mkataba wa mwaka mmoja
Bila shaka haitakuwa rahisi kwa Yanga kuwaachia nyota hao hasa ikizingatiwa mabingwa hao wa kihistoria nao wanakiimarisha kikosi chao ili kurejesha heshima waliyoipoteza misimu ya hivi karibuni
Yanga imepania kushiriki michuano ya CAF msimu ujao, ndio maana wameweka mkazo kushinda ubingwa wa ligi kuu na kombe la FA
Kama watafanikiwa ni wazi hawawezi kuwaachia nyota hao ambao ni tegemeo kikosini
Lakini pia Yanga iko kwenye mchakato wa mabadiliko kubadli mfumo wao wa uendeshaji lengo likiwa kujiendesha kibiashara zaidi
Ili kuvutia wawekezaji lazima timu ifanye vizuri, ni wazi watahitaji kuwa na wachezaji bora