Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msola jana aliongoza msafara wa viongozi na wachezaji wa timu hiyo kuuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17 Dar es Salaam
Wananchi wanakumbuka jambo kubwa ambalo hayati Magufuli aliwafanyia kupitia aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda, kwa kuwapatia eneo la ujenzi wa uwanja kule Kigamboni
Yanga inaendelea na mchakato wa kujenga kituo chake cha michezo (Yanga Complex) katika eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 7
Katika eneo hilo Yanga inatarajiwa kuwa na viwanja vya soka, Hostel, Gym na miundombinu mingine muhimu kwa ajili ya timu ya mpira wa miguu
Msafara wa Yanga uliofika uwanja wa Uhuru kutoa heshima zao za mwisho uliongozwa na Mwenyekiti Dk Msolla, lakini pia alikuwepo Mshauri Mkuu wa klabu Senzo Mbatha raia wa Afrika Kusini na baadaye Katibu Mkuu, Haji Mfikirwa na kocha wa muda wa kikosi hicho, Juma Mwambusi ambaye alikuwa mbele ya Meneja, Hafidh Saleh.
Wachezaji walioshiriki ni Zawadi Mauya, Haruna Niyonzima, Tuisila Kisinda, Waziri Junior, Yacouba Songne, Michael Sarpong na Fiston Abdul Razack
Dk Msola amesema watamkumbuka Magufuli kwa mambo mengi lakini muhimu zaidi pamoja na uzalendo wake wa Taifa, hayati Magufuli alikuwa mpenda michezo
"Kama klabu tumetoa heshima yetu kwa Hayati Rais John Magufuli ambaye wakati wake wa uongozi alikuwa mpenda michezo," alisema Dk Msolla.