Kiungo mshambuliaji wa Yanga Saido Ntibazonkiza kesho Ijumaa anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kuanza mazoezi ya timu
Ntibazonkiza alikuwa majeruhi tangu mwezi Januari, alijumuishwa kwenye timu ya Taifa ya Burundi, akianza na mazoezi mepesi
Kiongozi wa Shirikisho la Soka Burundi, amedokeza kuwa Ntibazonkiza atafanyiwa vipimo kesho Ijumaa kabla ya kujumuishwa katika mazoezi ya timu
Hata hivyo, amesisitiza kuwa wataendelea kumfuatilia kujiridhisha kama yuko fiti kwa asilimia 100 ili kuepuka kumuongezea majeraha
"Saido ameanza mazoezi mepesi tunategemea Ijumaa ataanza kuchezea mpira baada ya kufanyiwa vipimo tena kujiridhisha kwamba yuko sawa, ila tunaamini ikichelewa sana Jumatatu atakuwa uwanjani,β alisema kiongozi huyo
Burundi inajiandaa na mechi ya kufuzu Afcon dhidi ya Afrika ya Kati Ijumaa ijayo. Mchezo huo utapigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Aliyekuwa kocha wa Yanga Cedric Kaze alipinga Ntibazonkiza na beki Dickson Job kujumuishwa katika timu za Taifa kwa kuwa hawakuwa wamepona sawasawa
Kaze alisema kuwa wachezaji hao wanatibiwa na Yanga hivyo ni wao wanaofahamu hali zao huku akibainisha waliitiwa timu za Taifa pasipo uongozi wa Yanga kujulishwa
Kama Saido amepona kwa asilimia 100 ni habari njema kwa Yanga kuelekea ngwe ya lala salama ligi kuu ya Vodacom pamoja na mchezo wa kombe la FA dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa mwanzoni mwa mwezi wa nne