Mechi ya kilele cha wiki ya Mwananchi iliyopigwa August 04, 2020 ikiwa maalum kwa Yanga kukaribisha msimu wa 2020/21, ni miongoni mwa mechi ambazo Wananchi walicheza kiwango cha juu sana
Mchezo huo ambao Yanga ilishinda kwa mabao 2-0, Wananchi walionyesha ubora mkubwa licha ya kuwa timu ilikuwa pamoja kwa takribani wiki mbili tu
Ni Kocha Juma Mwambusi aliyekuwa akikinoa kikosi cha Yanga wakati huo akisubiriwa Zlatko Krmpotic
Baada ya Krmpotic kutua, ile kasi waliyoanza nayo ikapoa na haikushangaza kocha huyo kutimuliwa baada ya siku 37 tu
Cedric Kaze kwa kushirikiana na Mwambuzsi, akaja na mfumo tofauti ambao uliimarisha Yanga lakini nae pumzi zikamuishia baada ya kufanya mabadiliko ya kocha msaidizi, akimpendekeza Nizar Khalfan achukue nafasi ya Mwambusi
Hivyo hii ni mara ya pili msimu huu Mwambusi anarejea, sasa akikabidhiwa mikoba yote mpaka mwishoni mwa msimu
Hii ni nafasi kwake kuwaaminisha Wanayanga kuwa amestahili kuachiwa majukumu hayo na anaweza kuwapa furaha Wananchi kama alivyofanya katika mchezo wa wiki ya Wananchi
Wengi wanatamani kuiona Yanga ikirejea katika ushindani ule, kuwatoa hofu mashabiki na kufufua matumaini ya ubingwa
Tayari ameanza kwa kubadili program zote za mazoezi sasa vijana wakifanya mazoezi mara mbili kwa siku isipokuwa siku ya Ijumaa
Mwambusi anahitaji kupata dawa ya ubutu wa safu ya ushambuliaji, bila shaka eneo hili atalipa kipaumbele