Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Papy Kimoto, amepania kupata matokeo mazuri mbele ya waajiri wake wa zamani, AS Maniema Union ya DR Congo, katika mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF).
Kimoto amesema kikosi chake kinaendelea na maandalizi makali kuelekea mchezo huo utakaopigwa Jumapili, Novemba 29, 2026, nchini DR Congo, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia kila jambo ili kupata matokeo chanya ugenini.
Mchezo huo utakuwa wa kipekee kwa Kimoto kutokana na historia yake ya kuifundisha Maniema Union kwa miaka minne, kabla ya kutua Singida Black Stars. Kocha huyo ameeleza kufurahishwa na hatua iliyofikiwa na timu zote mbili katika mashindano hayo ya kimataifa.
Akizungumzia mwenendo wa kikosi chake, Kimoto amekiri kuwa matokeo yasiyotabirika ya Singida Black Stars yamechangiwa na changamoto za maandalizi ya awali ya msimu pamoja na usajili.
Hata hivyo, amesema kwa sasa kikosi chake kimeimarika kimwili na kimbinu, huku mipango ikiendelea ya kukiongezea nguvu kupitia dirisha dogo la usajili.
Kimoto ameweka wazi kuwa moja ya malengo yake makubwa ni kuiongoza Singida Black Stars kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, kama alivyowahi kufanya akiwa na Maniema Union.