MIKIKI mikiki ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC) inatarajiwa kutimua vumbi visiwani Zanzibar, wakati Azam FC itakapowakaribisha Al Ahly Tripoli ya Libya katika mchezo unaotarajiwa kuwa wa kukata na shoka.
Mtanange huo wa kwanza wa Kundi B utapigwa Ijumaa, Novemba 27, 2026, kuanzia saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Kikosi cha Azam FC kiliwasili visiwani Zanzibar jana kwa ajili ya kukamilisha maandalizi yake kuelekea mchezo huo muhimu, huku kikilenga kutumia vizuri faida ya kucheza nyumbani kuvuna pointi tatu za kwanza.
Kwa upande mwingine, wapinzani wao Al Ahly Tripoli nao tayari wamewasili visiwani humo, hali inayozidi kuongeza homa ya pambano hilo.
FISTON MAYELE AREJEA TANZANIA
Miongoni mwa mambo yanayoongeza mvuto wa mchezo huo ni uwepo wa mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Fiston Kalala Mayele, anayekipiga katika kikosi cha Al Ahly Tripoli.
Mayele si jina geni kwa mashabiki wa soka nchini Tanzania kutokana na makali aliyowahi kuyaonyesha wakati akiitumikia Yanga katika mashindano ya ndani na kimataifa.
Uwepo wa mshambuliaji huyo unaongeza changamoto kwa safu ya ulinzi ya Azam FC, ambayo itahitaji kuwa makini kuhakikisha haimpi nafasi ya kutumia uwezo wake wa kufumania nyavu.
AZAM FC YATAKA UWANJA UJAEE
Kuelekea mtanange huo, uongozi wa Azam FC umetoa wito kwa mashabiki wake visiwani Zanzibar kujitokeza kwa wingi kuijaza New Amaan Complex na kukipa nguvu kikosi chao.
Katika kuhakikisha mashabiki wengi wanapata fursa ya kushuhudia pambano hilo, viingilio vimepangwa kama ifuatavyo:
Mzunguuko – Sh 3,000
VIP B – Sh 5,000
VIP A – Sh 10,000
Azam FC inahitaji nguvu ya mashabiki katika mchezo huo, hasa kutokana na umuhimu wa kupata matokeo mazuri nyumbani katika hatua ya makundi ya michuano ya kimataifa.
POINTI TATU NDIZO HESABU ZA AZAM
Kwa Azam FC, kuanza kampeni ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa ushindi kutakuwa hatua muhimu katika kujenga mazingira mazuri ya kupigania tiketi ya robo fainali.
Hata hivyo, mbele yao wanasimama Al Ahly Tripoli, ambao nao watakuwa na dhamira ya kuondoka Zanzibar na matokeo chanya.
Tayari timu zote mbili zimetua visiwani Zanzibar, maandalizi yanaelekea ukingoni na sasa kilichobaki ni kusubiri dakika 90 za kazi.