Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo Duniani (CAS) imeirejeshea Senegal ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), baada ya kukubali rufaa iliyokatwa na Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) kupinga uamuzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Katika hukumu iliyotolewa leo, Novemba 24, 2026, CAS imebatilisha uamuzi wa Kamati ya Rufaa ya CAF na kurejesha matokeo ya awali ya mchezo wa fainali, ambapo Senegal iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Morocco.
Uamuzi huo unamaanisha kuwa Simba wa Teranga wamethibitishwa tena kuwa mabingwa wa Afrika, baada ya mvutano wa kisheria uliodumu kwa zaidi ya miezi kumi tangu mchezo huo wa fainali.
Chanzo cha mgogoro
Ikumbukwe kuwa fainali hiyo iliyochezwa Januari 18, 2026, jijini Rabat, nchini Morocco, iligubikwa na utata mkubwa baada ya mwamuzi Jean-Jacques Ndala kuipatia Morocco penalti katika dakika za nyongeza za muda wa kawaida.
Wachezaji wa Senegal waliondoka uwanjani kwa muda wakipinga uamuzi huo, kabla ya nyota wao Sadio ManΓ© kuwashawishi kurejea na kuendelea na mchezo.
Baada ya mchezo kurejea, kipa Edouard Mendy aliokoa penalti iliyopigwa na Brahim DΓaz, kabla ya Pape Gueye kufunga bao pekee la ushindi katika muda wa nyongeza na kuipa Senegal taji hilo.
CAS yabatilisha uamuzi wa CAF
Machi 17, 2026, Kamati ya Rufaa ya CAF ilibatilisha matokeo ya fainali hiyo kwa kutumia vifungu vya 82 na 84 vya kanuni za AFCON, ikiipa Morocco ushindi wa mabao 3-0 kwa hoja kwamba Senegal ilisusia mchezo.
Senegal haikuridhishwa na uamuzi huo na Machi 25, 2026, iliwasilisha rufaa yake mbele ya CAS yenye makao makuu jijini Lausanne, nchini Uswisi.
Miongoni mwa hoja za Senegal ilikuwa kwamba mwamuzi aliruhusu mchezo kuendelea hadi kukamilika, hivyo matokeo yaliyopatikana uwanjani yalipaswa kuheshimiwa.
Kesi hiyo ilisikilizwa Oktoba 8, 2026, mbele ya jopo la waamuzi watatu, kabla ya hukumu kutolewa leo kwa manufaa ya Senegal.
Senegal yathibitisha taji la pili
Kwa uamuzi huo, Senegal imerejesha taji lake la pili la AFCON katika historia, baada ya kutwaa ubingwa wake wa kwanza katika michuano ya mwaka 2021.
Hukumu hiyo ni ushindi mkubwa kwa Senegal katika vita vya kisheria na inaweka historia katika soka la Afrika, kufuatia moja ya migogoro mikubwa ya kimashindano iliyowahi kushuhudiwa katika fainali za AFCON.
Hatimaye, baada ya siku 310 za mvutano tangu fainali hiyo, ushindi wa Senegal wa bao 1-0 dhidi ya Morocco umerejeshwa na Simba wa Teranga wamethibitishwa tena kuwa mabingwa wa Afrika.