Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, ameshtukia mbinu za wapinzani wake wanaoonekana kujipanga kwa nguvu zaidi kila wanapokutana na timu hiyo, hali iliyomfanya kuona umuhimu wa kuongeza dozi ya maandalizi ili kuendeleza rekodi ya ushindi katika Ligi Kuu Bara.
Barker amebaini kuwa mwenendo mzuri wa Simba msimu huu umeongeza presha kwa wapinzani, ambao sasa wanaingia uwanjani wakiwa na dhamira ya kusimamisha kasi ya Wekundu wa Msimbazi, jambo linalofanya michezo kuwa migumu kadiri ligi inavyoendelea.
Simba imeweka rekodi ya kushinda michezo yote 11 iliyocheza hadi sasa, ikikusanya pointi 33 kati ya 33 zinazowezekana, lakini Barker anaamini mafanikio hayo yanahitaji kuambatana na maandalizi ya ziada, uimara wa kiakili na mbinu tofauti ili kuendelea kupata matokeo mazuri.
Akizungumzia hali hiyo baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya JKT Tanzania, Barker alisema changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa ni namna ambavyo kila mpinzani anajiandaa kwa lengo la kuwa timu ya kwanza kuivunja rekodi yao ya kutopoteza pointi.
"Ukiangalia katika mechi chache zilizopita unaweza kuona vile kumekuwa na changamoto kwa sababu kila timu ina lengo lake na inataka kuvunja mfululizo wetu wa ushindi. Tunachopaswa kufanya sisi kama timu ni kuendelea kuonyesha mentaliti imara na tabia ya kushinda," alisema Barker.
Kauli hiyo inaonyesha kuwa licha ya Simba kuendelea kupata ushindi, benchi la ufundi linatambua umuhimu wa kuongeza umakini katika maandalizi, hasa kutokana na namna wapinzani wanavyozidi kuwa wagumu na kutumia mbinu mbalimbali kuzuia mashambulizi ya timu hiyo.
Katika mchezo dhidi ya JKT Tanzania, Simba ililazimika kutoka nyuma baada ya kuruhusu bao la kwanza, kabla ya kupambana na kubadili matokeo na kuondoka na pointi tatu muhimu.
Barker alisema mazingira hayo yanadhihirisha uimara wa kikosi chake, akieleza kuwa wachezaji wamejenga tabia ya kutokubali kushindwa hata wanapokutana na upinzani mkali.
Kocha huyo alikumbusha kuwa tangu mwanzo wa msimu Simba imekuwa ikikabiliana na changamoto tofauti, ikiwemo kupata kadi nyekundu katika michezo mitatu ya kwanza, lakini bado ikaibuka na ushindi katika michezo yote licha ya kucheza ugenini.
"Tulianza msimu kwa kupata kadi nyekundu tatu katika michezo yetu mitatu ya kwanza, lakini tulishinda yote. Pia tumekuwa tukishinda baadhi ya mechi kwa tofauti kubwa, ikiwemo ushindi wa mabao 6-1. Hiyo inaonyesha tunaweza kushinda katika mazingira tofauti," alisema.
Mbali na mchezo dhidi ya JKT Tanzania, Simba imeonyesha uwezo wa kupambana katika mazingira magumu kwenye michezo mingine, ikiwemo ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga katika Dabi ya Kariakoo na ule wa mabao 3-2 dhidi ya Namungo baada ya kutoka nyuma.