Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, ameweka wazi kuwa kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya JKT Tanzania, utakaochezwa kesho Jumamosi, Novemba 21, katika Uwanja wa Isamuhyo, Mbweni, jijini Dar es Salaam.
Barker amesema ametumia vizuri kipindi cha mapumziko ya kalenda ya FIFA kukiandaa kikosi chake, huku akieleza kuwa wachezaji wake wana ari na morali ya kuhakikisha wanaendeleza mwenendo mzuri wa ushindi waliokuwa nao kabla ya ligi kusimama.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, kocha huyo amesema maandalizi yamekwenda vizuri, lakini amesisitiza umuhimu wa wachezaji wake kuingia uwanjani wakiwa na umakini mkubwa kutokana na ubora na ushindani wa JKT Tanzania.
"Maandalizi yanakwenda vizuri na tulianza kufanya hivyo wakati wa kalenda ya FIFA. Tunahitaji kuingia kwenye mchezo huu na umakini mkubwa.
"Lengo letu ni kupata ushindi ili kuendeleza matokeo mazuri tuliyokuwa nayo kabla ya mapumziko ya ligi," amesema Barker.
Hata hivyo, Barker ametambua kuwa mchezo dhidi ya JKT Tanzania hautakuwa mwepesi, hivyo amewataka wachezaji wake kutomchukulia mpinzani kwa urahisi ili kuepuka kupoteza pointi muhimu.
Kwa upande wake, kiungo wa Simba, Hussein Semfuko, akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, amesema kikosi hicho kimejipanga kikamilifu kupambana kuhakikisha kinapata alama zote tatu.
"Wachezaji tumejipanga vizuri kwa ajili ya kuzipambania pointi tatu. Kila mechi kwetu ni muhimu kupata pointi tatu licha ya ugumu wa mpinzani.
"Tunahitaji kushinda ili kuhakikisha msimu huu tunatimiza malengo ya kutwaa ubingwa," amesema Semfuko.
Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa na dhamira ya kuendeleza matokeo mazuri na kuimarisha nafasi yake katika mbio za ubingwa, huku JKT Tanzania ikitarajiwa kutoa upinzani mkali mbele ya wekundu hao wa Msimbazi.
Mchezo huo utakuwa mtihani mwingine muhimu kwa Steve Barker na vijana wake katika safari ya kutimiza malengo ya Simba ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.