Timu ya taifa ya Ureno imepanga kutoa heshima maalumu kwa nahodha wake wa muda mrefu Cristiano Ronaldo katika mchezo wake ujao dhidi ya Denmark, kufuatia taarifa za kustaafu kwake soka la kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, wachezaji wote wa Ureno wanatarajiwa kuingia uwanjani wakiwa wamevaa jezi yenye namba 7, ambayo imekuwa alama ya utambulisho wa Ronaldo katika timu hiyo. Aidha, mchezo huo utasimamishwa kwa muda dakika ya 7 ili kutoa heshima kwa mshambuliaji huyo.
Hatua hiyo inaripotiwa kufikiwa baada ya Bernardo Silva, Ruben Dias na Bruno Fernandes kukutana na benchi la ufundi pamoja na rais wa Shirikisho la Soka la Ureno kujadili namna bora ya kumuenzi Ronaldo.
Mbali na heshima hiyo uwanjani, Ureno pia inaripotiwa kupanga kutotumia tena chumba namba 201 katika kambi ya timu ya taifa, ambacho Ronaldo alikuwa akikitumia wakati wa maandalizi ya mechi. Chumba hicho hakitapangiwa mchezaji mwingine.
Ronaldo anaondoka katika timu ya taifa akiwa na rekodi ya kipekee ya kuwa mfungaji bora wa muda wote katika soka la kimataifa, akiwa amecheza mechi 234, kufunga mabao 146 na kutoa pasi 37 zilizozaa mabao. Heshima hizo zinatarajiwa kuwa sehemu ya kumuenzi mchezaji aliyeacha alama kubwa katika historia ya soka la Ureno.