Nahodha na kiungo wa Manchester United, Bruno Fernandes, ameripotiwa kukataa ofa ya pili iliyoboreshwa ya mkataba mpya kutoka kwa uongozi wa klabu hiyo, hatua inayozidi kuongeza mashaka kuhusu mustakabali wake katika dimba la Old Trafford.
Taarifa zinaeleza kuwa kiungo huyo raia wa Ureno bado hajaridhishwa na masharti ya mkataba aliowekewa mezani, hususan suala la mshahara na muda wa makubaliano hayo. Mbali na maslahi ya kifedha, mwenendo wa klabu hiyo na matarajio yake ya mafanikio ya kisoka pia yanatajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayoweza kuathiri uamuzi wake.
Fernandes ana mkataba na Manchester United hadi Juni 2027, huku klabu ikiwa na kipengele cha kuongeza muda wa mkataba huo kwa mwaka mmoja zaidi. Hata hivyo, kukataliwa kwa ofa mbili mfululizo kunaongeza presha kwa uongozi wa United kutafuta suluhisho kuhusu hatma ya nahodha huyo.
Hali hiyo inakuja wakati Manchester United ikiendelea kupitia kipindi cha mabadiliko ya kiufundi na kutafuta utulivu wa matokeo. Fernandes ni mmoja wa wachezaji muhimu katika kikosi hicho, hivyo uwezekano wa kuondoka kwake unaweza kuwa pigo kwa mipango ya klabu katika misimu ijayo.