Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeridhia Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kutumika kwa michezo ya kimataifa ya klabu za Simba SC na Young Africans katika hatua za makundi za Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2026/27, baada ya kukamilika kwa maboresho yaliyokuwa yakihitajika ili kukidhi vigezo vya mashindano hayo.
Idhini hiyo ni habari njema kwa miamba hiyo ya soka nchini, ambayo ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya kupata uwanja wa kuchezea michezo yake ya nyumbani baada ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kufungwa kwa ajili ya ukarabati. Awali, Simba na Yanga zilikuwa zimeelekeza macho yao kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, kama mbadala wa kuchezea mechi zao za kimataifa.
Hata hivyo, Uwanja wa Uhuru ulikuwa na baadhi ya mapungufu yaliyohitaji kurekebishwa ili uweze kukidhi viwango vya CAF. Kukamilika kwa maboresho hayo na kuridhiwa na chombo hicho cha soka barani Afrika sasa kunatoa suluhisho la changamoto iliyokuwa ikiikabili timu hizo mbili.
Kwa upande mwingine, Uwanja wa New Amaan Complex nao unatarajiwa kufungwa kwa ajili ya maboresho zaidi baada ya mchezo wa Taifa Stars dhidi ya Nigeria unaotarajiwa kuchezwa Novemba 17, jambo linaloendelea kuonyesha umuhimu wa maandalizi ya miundombinu ya michezo nchini kuelekea AFCON 2027.
Uamuzi huo unatarajiwa kuwaondolea Simba na Yanga usumbufu wa kusafiri kwenda Zanzibar kwa ajili ya michezo yao ya nyumbani ya kimataifa, huku mashabiki wa timu hizo wakipata nafasi ya kuziunga mkono moja kwa moja jijini Dar es Salaam.