Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Idd Suleiman 'Nado', ameongezwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kinachoelekea nchini Nigeria kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Nado, ambaye awali hakuwa amejumuishwa katika orodha ya wachezaji walioitwa kuunda kikosi cha Taifa Stars, hatimaye amepata nafasi ya kujiunga na timu hiyo kuelekea mchezo huo muhimu dhidi ya Super Eagles ya Nigeria.
Kuongezwa kwa kiungo huyo kunakuja wakati kukiwa na maoni mbalimbali kutoka kwa wadau wa soka nchini waliokuwa wakipendekeza ajumuishwe kikosini kutokana na kiwango kizuri anachokionyesha akiwa na klabu yake ya Azam FC.
Msimu huu, Nado amekuwa na mchango mkubwa katika kikosi cha matajiri hao wa Chamazi, akifanikiwa kufunga jumla ya mabao matano katika mashindano yote aliyoshiriki.
Uwezo wake wa kucheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, kutengeneza nafasi na kuchangia mabao unaweza kuongeza chaguo katika safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars kuelekea mtihani huo dhidi ya Nigeria.