Tanzania imepata ahueni kuelekea michezo ya kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 dhidi ya Nigeria baada ya mshambuliaji tegemeo wa Super Eagles, Victor Osimhen, kuthibitishwa kukosa michezo hiyo kutokana na jeraha la goti la kushoto.
Osimhen, ambaye ni miongoni mwa washambuliaji muhimu wa kikosi cha Nigeria, alipata jeraha hilo wakati klabu yake ya Galatasaray ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya VfB Stuttgart katika mchezo wa UEFA Champions League.
Kwa mujibu wa taarifa, vipimo vya MRI vilibaini kuwa mshambuliaji huyo ana tatizo kwenye goti lake la kushoto, huku akitarajiwa kufanyiwa upasuaji mdogo wa aina ya arthroscopy katika Hospitali ya Maslak Acbadem nchini Uturuki.
Inakadiriwa kuwa Osimhen atakuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki mbili hadi tatu huku akiendelea na matibabu na kurejesha utimamu wake wa mwili.
Kutokana na hali hiyo, nyota huyo atakosa michezo miwili ya kufuzu AFCON 2027 dhidi ya Tanzania, pamoja na mchezo wa Galatasaray dhidi ya Amed SK.
Kukosekana kwa Osimhen ni pigo kwa Nigeria kutokana na mchango wake mkubwa katika safu ya ushambuliaji. Hata hivyo, kwa upande wa Tanzania, taarifa hiyo inaweza kuwa ahueni kuelekea michezo hiyo muhimu, kwani Taifa Stars haitakabiliana na mmoja wa washambuliaji hatari zaidi wa Super Eagles.
Stars na Nigeria zitachuana Novemba 13 (Lagos) na Novemba 17 (Zanzibar).