Kocha Mkuu wa Namungo FC, Juma Mgunda, amesema atatumia mafunzo aliyoyapata katika mchezo dhidi ya Simba SC kurekebisha mapungufu ya kikosi chake na kukiimarisha zaidi kwa ajili ya michezo ijayo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Namungo ilikubali kichapo cha mabao 3-2 dhidi ya Simba katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, lakini licha ya matokeo hayo, Mgunda amesema mchezo huo umempa nafasi ya kujifunza mambo muhimu yatakayosaidia kuboresha timu yake.
Akizungumzia mchezo huo, Mgunda amekiri kuwa Simba ni timu yenye wachezaji wenye ubora na uwezo mkubwa, huku akiwapongeza kwa kiwango walichoonesha katika mchezo huo.
"Simba ni timu kubwa na ina wachezaji wenye uwezo mkubwa pia. Ukikutana na timu ya aina hii hupaswi kufanya makosa mengi kwani wanaweza kukuadhibu kwa kila kosa unalofanya."
"Tumejifunza na tutatumia mechi hii kama funzo kwetu ili kuhakikisha tunakuwa bora zaidi kwenye michezo ijayo," alisema Mgunda
Simba ilitangulia kufunga kwenye mchezo huo kupitia kwa ANicet Oura kabla ya Raymond Lulendi kufunga mabao mawili yaliyopa uongozi Namungo Fc.
Hata hivyo dakika 11 za mwisho zilikuwa ngumu kwao, Simba ikisawazisha na kufunga bao la ushindi dakika ya 88 kupitia Oura aliyekuwa nyota wa mchezo huo