Kiungo wa Everton, Jack Grealish, ameripotiwa kutumia usiku mbili mfululizo akiburudika katika kumbi za starehe siku chache kabla ya kuondolewa kwenye kikosi cha timu hiyo kutokana na suala la kinidhamu.
Kwa mujibu wa gazeti la The Sun, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 na mshahara unaoripotiwa kuwa pauni 300,000 kwa wiki, alionekana akiburudika Oktoba 19 na 20.
Usiku wa kwanza, Grealish alihudhuria hafla ya Pride of Britain Awards jijini London kabla ya kuelekea katika ukumbi wa karaoke ambako alikaa hadi majira ya asubuhi.
Siku iliyofuata alirejea eneo la North West na kuhudhuria mazoezi ya Everton, lakini jioni yake alitoka tena kwenda katika baa ya The Mucky Pup iliyopo Wilmslow.
Katika tukio hilo, aliripotiwa kuwa pamoja na wachezaji wenzake wa Everton, Jordan Pickford na Tyler Dibling, pamoja na Kyle Walker, aliyewahi kucheza naye Manchester City. Kundi hilo lilitazama mchezo wa PSG dhidi ya Barcelona katika chumba maalumu huku likiburudika.
Siku chache baadaye, Grealish hakuwepo kwenye kikosi cha Everton kilichoshinda dhidi ya Newcastle katika Carabao Cup, jambo lililozua maswali kuhusu sababu za kuachwa kwake.
Kocha wa Everton, David Moyes, alipoulizwa kuhusu uamuzi huo alisema: “Klabu ilifanya uamuzi huo na ninauunga mkono.”
Hata hivyo, taarifa za The Sun zinaeleza mazingira yaliyozunguka tukio hilo, huku klabu ikieleza kuwa uamuzi wa kumwacha mchezaji huyo ulitokana na suala la kinidhamu.