Shirikisho la Soka Afrika CAF linatarajiwa kufanya droo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika leo, huku timu kutoka Tanzania zikisubiri kufahamu wapinzani wao katika hatua hiyo.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba SC na Young Africans zipo kwenye poti ya pili, pamoja na Al Hilal ya Sudan na Petro de Luanda ya Angola. Timu hizo zitapata wapinzani kutoka katika makapu mengine, huku Orlando Pirates ya Afrika Kusini ikiwa kwenye kapu la tatu.
Poti ya kwanza lina Espérance de Tunis, RS Berkane, Pyramids FC na Zamalek SC. Poti ya tatu lina MC Alger, Orlando Pirates, FC Nouadhibou na Horoya AC, wakati poti ya nne lina Club Africain, Wiliete SC, Colombe Sportive na Maghreb de Fès.
Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC na Singida Black Stars ndizo timu za Tanzania zilizopo kwenye kapu la pili na la tatu mtawalia. Azam FC itasubiri kufahamu wapinzani wake kutoka makapu mengine, huku Singida Black Stars nayo ikitarajia kupata changamoto mpya katika hatua hiyo.
Poti ya kwanza lina Al Ahly, USM Alger, AS FAR na mshindi wa mchezo kati ya CR Belouizdad dhidi ya Douanes/Hafia. Poti ya pili lina Raja Club Athletic, AS Maniema Union, Azam FC na CS Sfaxien.
Poti ya tatu lina Al Ahli Tripoli, Singida Black Stars, Black Bulls na Real Bamako. Poti ya nne lina AS Kara, Durban City, Red Arrows na 1º de Agosto.
Droo ya Ligi ya Mabingwa Afrika inatarajiwa kuanza saa 7:00 mchana kwa saa za Afrika Mashariki kupitia CAF TV kwenye YouTube. Mashabiki wa soka wanasubiri kuona timu za Tanzania zitapangwa katika makundi yapi na zitakutana na wapinzani gani katika safari ya kuwania mataji ya Afrika.