Barcelona imezindua jezi maalumu itakayotumika katika El Clasico dhidi ya Real Madrid Oktoba 25, 2026, ikiwa na nembo ya GOLF WANG ya msanii wa Marekani Tyler, The Creator, badala ya nembo ya kawaida ya Spotify kwenye sehemu ya mbele ya jezi. Uzinduzi huo ni sehemu ya ushirikiano kati ya Barcelona, Spotify na chapa ya mavazi ya msanii huyo.
Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Barcelona kufanya mabadiliko ya aina hiyo katika mchezo dhidi ya Real Madrid. Klabu hiyo imekuwa ikitumia jezi zenye nembo maalumu za wasanii mbalimbali katika El Clasico kupitia ushirikiano wake na Spotify, hatua iliyolenga kuunganisha muziki, mitindo na soka.
Tyler, The Creator anakuwa msanii wa tisa kushirikiana na Barcelona katika kampeni ya jezi maalumu za El Clasico, utamaduni ulioanza mwaka 2022 kwa ushirikiano na Drake. Wasanii wengine waliohusika katika kampeni zilizopita ni Rosalía, The Rolling Stones, Karol G, Coldplay, Travis Scott, Ed Sheeran na Olivia Rodrigo.
Barcelona imetangaza kuwa jezi hizo zitapatikana kwa matoleo maalumu, likiwemo toleo lenye nakala 1,899. Mbali nnaomna jezi, ushirikiano huo utahusisha mkusanyiko wa mavazi na bidhaa mbalimbali zenye muundo wa GOLF WANG, zikiwemo jaketi, fulana, hoodies, soksi na skafu.
Jezi hiyo itaanza kuvaliwa na timu ya wanawake ya Barcelona katika mchezo dhidi ya Granada Oktoba 24, kabla ya kikosi cha wanaume kuitumia siku inayofuata katika pambano la El Clasico dhidi ya Real Madrid kwenye Spotify Camp Nou. Kwa mara ya kwanza katika ushirikiano wa aina hii, Tyler, The Creator pia amehusika moja kwa moja katika ubunifu wa kampeni ya picha na video.
.jpg.jpg)