Zanzibar imeingia makubaliano ya ushirikiano na Real Madrid Foundation pamoja na Unicorn Zanzibar Sports Limited kwa lengo la kukuza vipaji vya soka kwa vijana, kuimarisha nidhamu na kujenga maadili kupitia mfumo wa mafunzo unaozingatia viwango vya kimataifa.
Hayo yamesemwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Jumanne, Oktoba 13, 2026, jijini Madrid, Uhispania, wakati wa hafla ya kusaini Hati ya Makubaliano. Mpango huo unatarajiwa kuanza kwa programu maalumu za mafunzo ya soka kwa vijana, kabla ya kuanzishwa kwa akademia ya kudumu katika Viwanja vya Michezo Zanzibar.
Katika hafla hiyo, Dkt. Mwinyi alipokea jezi ya Real Madrid kutoka kwa Roberto Carlos, nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil na balozi wa klabu hiyo, pamoja na Julio González Ronco, Mkurugenzi wa Real Madrid Foundation. Rais Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya michezo na mifumo ya mafunzo ili kuwawezesha vijana kukuza uwezo wao.
Ameeleza kuwa Zanzibar tayari imeendeleza zaidi ya viwanja 30 vya mpira wa miguu, akisisitiza kuwa mafanikio ya michezo yanahitaji kuunganisha vipaji, elimu, nidhamu na makocha wenye weledi.