Siku mbili baada ya kukamilika kwa Dabi ya Kariakoo ambapo Simba SC iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga SC, tambo za nje ya uwanja zimechukua sura mpya.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, amezua sintofahamu mtandaoni baada ya kuchapisha picha ya sindano na kuacha maswali yanayodokeza kuwa watani wao walitumia mbinu haramu (sindano za kuongeza nguvu) kupata ushindi huo uwanjani.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Kamwe aliandika ujumbe mzito uliosomeka:
“Jiulize kwanini inatumika nguvu kubwa hivi hadi kuunganisha wasemaji waje kutetea Timu yao na kutukana watu kama jambo sio la kweli? Jiulize kwanini inatumika nguvu kubwa 'Kutetea Ushindi' na sio 'kufurahia ushindi'? Ukweli hauko mbali,” aliandika Kamwe
Hatua hiyo imetafsiriwa na mashabiki wengi kama tuhuma dhidi ya Simba kutokana na kasi na nguvu kubwa waliyoonyesha wachezaji wao wakati wa mchezo huo.
Simba SC wafunguka, wapinga vikali
Akijibu tuhuma hizo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, pamoja na Kocha Mkuu wao, Steve Barker, wameibuka na kupinga vikali madai hayo wakisema ni visingizio vya kushindwa.
Kocha Steve Barker amesisitiza kuwa uwezo mkubwa ulioonyeshwa na kikosi chake kurejea mchezoni na kupata ushindi ni uthibitisho wa maandalizi mazuri na ubora wa mbinu zao uwanjani, na si mambo ya kubahatisha.
Upande wa viongozi na wachambuzi wa soka umewataka Yanga kukubali matokeo, huku wengi wakikumbusha kuwa Simba ilikuwa haijapata ushindi wa dabi kwenye Ligi Kuu kwa kipindi cha miaka mitatu na miezi mitano, hivyo ushindi huo ulikuja kwa haki kutokana na jasho lao.
Mchezo huo uliomalizika kwa Simba kushinda 2-1 umeendelea kuacha sintofahamu kubwa, huku wadau wa soka nchini wakisubiri kuona kama Bodi ya Ligi (TPLB) au Kamati ya Maadili ya TFF itaingilia kati sakata hili la tuhuma za "sindano" ili kulinda taswira na maadili ya soka la Tanzania.