Kocha Mkuu wa Coastal Union, Fikiri Elias, amesema anatarajia mchezo mgumu dhidi ya Azam FC watakaowakaribisha kesho, Ijumaa, Oktoba 9, 2026, kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, ametoa kauli ya tahadhari na heshima kuelekea mchezo huo wa Ligi Kuu ya NBC, akisisitiza kuwa hakuna mchezo mwepesi katika ligi hiyo kwa sasa.
Ibenge amesema amekuwa akisisitiza nidhamu kwa wachezaji wake, akitambua kuwa kila mpinzani anayekutana nao huingia uwanjani akiwa na morali kubwa ya kupambana.
Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Zidane Sereri, amewaahidi mashabiki wa timu hiyo ushindi kuelekea mchezo huo dhidi ya Coastal Union.
Naye kipa wa Coastal Union, Khatibu Mwakisiki, amesema kocha wao, Fikiri Elias, amewapa mbinu za kukabiliana na Azam FC ndani ya dakika 90 za mchezo huo.
Mwakisiki amesema endapo watafuata maelekezo ya kocha wao, anaamini wataibuka na ushindi katika mchezo huo unaotarajiwa kuanza saa 3:00 usiku kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.