Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefafanua kuhusu wachezaji wa klabu waliopo kwenye kambi ya Taifa Stars waliopatiwa ruhusa kurejea kwenye timu zao, likisema si Yanga SC pekee iliyoomba kurejeshewa wachezaji wake.
TFF imesema Yanga SC, Simba SC na Singida Black Stars zote zimewasilisha maombi ya kurejeshewa wachezaji wao kutoka kwenye kambi ya Taifa Stars, na maombi hayo yamekubaliwa.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa TFF, Evans Mgeusa, kufuatia taarifa zilizoibuka zikidai kuwa ni wachezaji wa Yanga SC pekee waliopewa ruhusa kuondoka kambini.
Mgeusa amefafanua kuwa Yanga SC iliwasilisha ombi lake mapema, huku Simba SC na Singida Black Stars zikiwasilisha maombi yao siku iliyofuata.
“Yanga SC wao waliomba tangu Septemba 30, 2026, ila Simba SC na Singida Black Stars wao wameomba jana, Oktoba 1, 2026, na wote tumewaruhusu,” alisema Mgeusa.
Kwa mujibu wa Mgeusa, wachezaji wa Yanga SC walitarajiwa kuondoka kambini Oktoba 3, 2026, wakati Simba SC na Singida Black Stars zilikuwa bado hazijakamilisha taratibu za safari za kuwarejesha wachezaji wao nchini.
“Wachezaji wa Yanga SC wanaondoka kesho (leo), hao ndio najua. Ila Simba SC na Singida BS bado timu zao hazijakata tiketi ili tujue ni lini wanaondoka kambini kurudi Tanzania,” aliongeza.
Stars kuendelea na maandalizi Morocco
Taifa Stars iko nchini Morocco kwa ajili ya michezo ya kirafiki, baada ya kukamilika kwa mechi mbili za kuwania kufuzu AFCON 2027.
Stars inatarajiwa kushuka dimbani Oktoba 5, 2026, dhidi ya wenyeji Morocco katika mchezo huo wa kirafiki.
Jana ilicheza dhidi ya AS FAR ya kukubali kipigo cha mabao 5-0